Katika ajali hiyo iliyotokea juzi saa 12:00 jioni katika Kitongoji cha
Kibiti Tarafa ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Mark II hiyo
yenye namba za usajili T. 363 AZG, iligongana uso kwa uso na Fuso yenye
namba za usajili T. 433 AYQ.
Ajali hiyo ilitokea wakati Mark II iliyokuwa ikiendeshwa na Abuu Ahmed
(21), kuwa katika mwendo kasi ikitokea Tanga kuelekea Morogoro kujaribu kulipita
Fuso lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Dar es Salaam likiendeshwa na Mweta
Daniel.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Gregory Mushi, alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa waliokufa katika ajali hiyo ni wanafunzi
wanne wa Shule ya Sekondari Chalinze wote wakazi wa eneo la Msolwa.
Aliwataja kuwa ni Essau Enos (16) wa kidato cha tatu, Latifa Shabani (17),
wa kidato cha nne, Bahati George (18), wa kidato cha nne na Stella Isaack
Kazimoto, (18).
Aliwataja watu wengine waliofariki dunia wakiwa katika Mark II kuwa ni
Hassan Kulunga na Maria Sadick, wakazi wa Ubena ambao umri wao haukufahamika
mara moja. Wengine ni dereva wa Mark II, Abuu Ahmed (21) na mtoto anayekadiriwa
kuwa na umri wa kati ya miaka minne na mitatu aliyefahamika kwa jina la Samwel
Ismail, ambaye ni mtoto wa marehemu, Maria Sadick. Aidha, Kaimu Kamanda huyo
aliwataja majeruhi waliokuwa wamepanda Fuso kuwa ni William Thobias (30), mkazi
wa Matombo mkoani Morogoro na utingo, Ahamad Juma (36).
Mushi alisema majeruhi hao wanaendelea na matibabu katika kituo cha afya
Chalinze na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi
wilayani Kibaha. Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Tumbi, Rose Mtei, alithibitisha
kupokea miili minane iliyokuwa imeharibika.
Kufuatia ajali hiyo, Kamanda Mushi ametoa wito kwa madereva kuzingatia
sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokea kwa uzembe na kwamba
Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani litawachukulia sheria kali madereva hao.
Shuhuda wa ajali hiyo, Godfrey Bonny, alisema ajali hiyo ilitokea wakati
dereva wa Mark II akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake ndipo gari lake
lilipokutana uso kwa uso na Fuso.
“Mimi ni mkazi wa Chalinze, ilikuwa ni saa 12:30 jioni, nilisikia kishindo
kikubwa na ndipo tulipokwenda katika eneo la tukio na kukuta gari dogo
limeharibika vibaya na ikiwa chini ya uvungu wa gari kubwa. Lakini kutokana na
kuchelewa kwa Kikosi cha Uokoaji, watu waliokuwamo ndani walipoteza maisha kwa
kukosa msaada wa haraka,” alisema Bonny.
Shuhuda mwingine, Yusuph Mjema, ambaye pia ni mkazi wa Chalinze, alisema
alipofika eneo la tukio, alikuta watu hao wamebanwa, lakini kutokana na kukosa
vifaa maalum kwa ajili ya uokoaji, ilichukua muda mrefu kuwatoa.
No comments:
Post a Comment